Alhamisi, 28 Mei 2015

JE UNAFAHAMU UMUHIMU WA SAIKOLOJIA YA ELIMU? SOMA HAPA


Saikolojia ya elimu ni tawi la taaluma ya saikolojia linaloshughulikia masuala ya elimu, tawi hili linachunguza jinsi mwanafunzi anavyojifunza mambo mbalimbali ya kielimu, kijamii na kiutamaduni na namna bora ya kumfundisha. Sasa hebu tuangalie tawi hili lina umuhimu gani? Au kuna umuhimu gani wa mwalimu kujua saikolojia?

Umuhimu wa saikolojia ya Elimu
1).Hii humsaidia mwalimu kujua tabia za mwanafunzi na kujua ni kwa njia au mbinu gani anaweza kuzitumia ili tendo la kujifunza litokee na pia kujua sababu zinazoweza kufanya tendo la kujifunza lisiimarike mfano wanafunzi hutofautiana sana kutokana na malezi waliyolelewa au mahala walipotokea, hivyo kama mwalimu ukishajua tofauti hizi utajua utumie mbinu zipi ili kuhakikisha kuna usawa wa elimu au ulichokifundisha kimeeleweka kwa wote bila ya kubagua mwenye uwezo mkubwa au mdogo.
2) Husadia pia kujua jinsi ubongo au akili ya binadamu inavyotumika katika tendo la kujifunza. Kujua huku kutafufua njia na mbinu mbalimbali kuhakikisha kinachofundishwa kimefanikiwa.
3) Husaidia kumjua vema mwanafunzi wako na kujua jinsi gani utamsaidia ili ajifunze vema zaidi.
4) Itakusaidia kufahamu matatizo yanayokwamisha mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji na kujua jinsi gani utaweza kuyatatua.
5) Kwa kufahamu saikolojia na tabia za wanafunzi wako utaweza kuwaandaa vema na kuwapa motisha ili walipende somo na kuwachochea inapobidi. Mfano unaweza kutumia mifano mizuri ya kile wanafunzi wanachokipenda ili kuwafanya wawe na furaha na umakini na kile unachokifundisha.
6) Utajua kama mwanafunzi ameelewa au hajakuelewa hata kama amekaa kimya bila ya kukuuliza au kusema lolote. Kuna wanafunzi huwa na uoga wa kuuliza swali pale anaposhindwa kuelewa sehemu fulani, hivyo kama una ujuzi wa saikolojia hali hii unaweza kuigundua kwa wanafunzi wako na kuirekebisha.

Kwa upande wangu nina hayo machache, ikiwa una lolote la kuongezea jisikie huru kuacha maoni yako kwani tuko pamoja katika kuelimisha jamii katika mambo mbalimbali.

0 maoni:

Chapisha Maoni