Alhamisi, 28 Mei 2015

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA


Ndugu wana UDPSA na wengine Makala hii itatusaidia Kujifunza kuhusu Saikolojia. Wengi kati ya watu wanaosumbuliwa na matatizo yanaoitwa ya dunia ni wale wanaopambana na nguvu zao bila kujua. Kwa kutumia akili zao vibaya, hujitesa kwa kufikiri na kutafsiri vibaya matukio ya kila siku yanayotokea duniani.

Kwa mfano, tukizungumzia kufa ambapo watu wengi wanaamini kwamba ni jambo baya, kuna wengine wanaona ni zuri ndiyo maana wapo wanaojiua, na kama tukisema vita ni hatari, bado kuna watu wanafurahia vita kwa vile si wote wanaowahurumia wafao vitani hata kama wataona maiti zao barabarani kwa wingi.
Kama nilivyosema, duniani kuna nguvu mbili, ambazo ni za watu wenyewe na za ulimwengu, hii ina maana kuwa hata mawazo ya mwanadamu ni nguvu na mtu anaposumbukia kuwaza jambo fulani kwa undani kiasi cha kuumiza moyo wake anakuwa anashindana na nguvu zake mwenyewe.
Ifahamike kuwa kadiri mwanadamu anavyozidi kuongeza nguvu ya kufikiri, iwe kwa kukua kimwili, kusoma na kujifunza mambo mengi zaidi, kwa asili anakuwa anaongeza nguvu ambazo asipokuwa makini anaweza kufa akishindana nazo badala ya kuzitumia katika kumsaidia kimaisha.
Kwa mfano, watu kutoka kabila la Wabarabeigi wanaopatikana mkoani Manyara, nchini Tanzania wanaishi maisha ya kuwinda wanyama na kula mizizi ya porini, hawawezi kukaa wakifikiri jinsi ya kupata gari kwa kuwa kwao gari halina maana. Kwao maendeleo ni kuwinda na kuzaliana.
Kwa maana hiyo linapokuja suala la maisha magumu litatokana na ukame na wala si ukosefu wa mitaji au kazi. Hawa hawawazi magari kwa sababu hawajajifunza umuhimu wake, hawajui umuhimu wa kuwa na zahanati, hospitali na wala bei ya mafuta haiwasumbui. Lakini kwa Wachaga waliozoea umeme wakikosa huduma hiyo kwao hilo litakuwa ni tatizo kubwa litakalowakosesha usingizi.
Vivyo hivyo, kwa watu waliozoea kutibiwa kwa sindano na vidonge, wakikosa tiba hizo itakuwa rahisi kwao kufa, kwa sababu akili zao zinatafsiri ukosefu huo kama tatizo kubwa kwao, lakini haiwi hivyo kwa Wasukuma wanaoishi maporini kusikokuwa na hospitali za rufaa wala umeme.
Tafsiri ya hili ni nini? Ni fikra zitokanazo na kujua mambo na namna ya kuyawaza. Watu wengi siku hizi wanajua utajiri, wanafahamu nini maana ya afya, wanaelewa umuhimu wa maendeleo lakini siyo wote wenye uwezo wa kukutana na changamoto hizo na kupata matokeo sahihi ya kile wanachokifahamu.
Kwenda hospitali kupimwa na kuambiwa kuwa una Kansa, Ukimwi, Kisukari, Pumu, TB na magonjwa kama hayo, siyo jambo linalowasaidia wengi kwa vile hawajui hatua ya kuelekea kwenye ujuzi huo wa mambo. Hapa ndipo elimu ya saikolojia inapohitajika ili iweze kumsaidia mtu anayejua mambo hayo namna ya kuyakabili, kuyaendeleza na kupata mafanikio.
Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wanaofahamu mambo hawafaidiki nayo na pale wanapojaribu kutumia ujuzi wao walioupata shuleni, wanajikuta wanaingia kwenye mapambano ya nguvu ya vile wanavyovifahamu.
Watu wengi leo hawalali usiku kucha wakipambana na yale waliyoyafahamu, utakuta mtu kakonda kwa sababu katambua mpenzi wake si mwaminifu, anakesha akilia bila kujua afanye nini kumaliza tatizo.
Mtu mwingine anakonda kwa sababu ni maskini, hana mtaji na ajabu nyingine kuna wanaosumbukia hata kasoro za maumbile yao ambazo wameumbwa nazo!

0 maoni:

Chapisha Maoni